Nothing Special   »   [go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Msalaba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Msalaba wa Kigiriki juu ya Msalaba wa Mt. Andrea.

Msalaba ni ishara inayotokana na mistari miwili kukutana katikati yake.

Hiyo ni mojawapo kati ya ishara maarufu na ya zamani zaidi duniani kote, katika sanaa, utamaduni na dini, hasa Ukristo unaoheshimu kama ukumbusho wa kifodini cha mwanzilishi wake, Yesu Kristo, aliyekufa kwa njia ya usulubisho.

Msalaba ulikwishatumiwa na Wakristo wa kale sana. Mwanzoni mwa karne ya 3 Tertullianus, katika kitabu "De Corona", alisema kwamba walikuwa na desturi ya kujifanyia ishara hiyo katika paji la uso.

Lakini alama ya msalaba au za kufanana na msalaba zinapatikana pia katika tamaduni mbalimbali tangu kale bila uhusiano wowote na Ukristo.

Misalaba iliyotumiwa kwa adhabu ya kifo iliweza kuwa na maumbo mbalimbali, hata kuwa ubao mmoja tu bila mikono ya kando.

Misalaba mbalimbali

[hariri | hariri chanzo]
Picha Jina la Msalaba Maelezo
Msalaba wa Misri ya Kale

Ankh au msalaba wa Misri; ni ishara kutoka utamaduni wa Misri ya Kale na ni ya kale zaidi kuliko msalaba wa Kikristo. Kwa Wamisri ilikuwa ishara ya uhai na uzao. Baadaye ilitumiwa pia katika sanaa ya Wakristo. Unajulikana pia kwa jina la Kilatini crux ansata ("msalaba wenye mikono").

Msalaba wa Kikristo

Umbo hili linajulikana pia kama msalaba wa Kilatini. Ni ishara itumiwayo na Wakristo wengi kama kumbukumbu ya Yesu Kristo na kifo chake kwa njia ya usulubisho na pia ufufuko wake.

Msalaba wa Jua , Msalaba wa Kibulgaria

Huu ni ishara ya kale kabisa inayopatikana tangu zamani za zama za mawe. Unaaminika kumaanisha jua. Katika sanaa ya Kikristo ulipatikana hasa Bulgaria kama ishara ya Kanisa la Bulgaria. Siku za nyuma imetumiwa pia na Wapagani wa kisasa.

Msalaba wa Kikelti

Unapatikana katika sanaa ya Wakristo Wakelti hasa Eire na pia katika sehemu kadhaa za kisiwa cha Britania kama msalaba juu ya makaburi na katika makanisa.

Msalaba wa Canterbury

Unapatikana hasa katika makanisa ya Kianglikana.[1]

Msulubiwa

Ni msalaba wenye sanamu ya mwili wa Yesu juu yake.

Msalaba wa Kiserbia (Msalaba wenye herufi nne kandokando)

Unatokana na bendera ya Konstantino Mkuu na kupatikana katika sarafu za Bizanti kuanzia karne ya 6. Kuanzia Karne za kati umetumiwa na nchi ya Serbia na Kanisa lake la Kiorthodoksi. Hadi leo ni kitambulisho cha taifa hilo.


Msalaba wa Mt. Floriano

Unatumiwa na zimamoto kutokana na msimamizi wao Floriani. Unafanana na ule wa Malta isipokuwa ncha za mikono yake ni za mviringo.

Msalaba wa Mashariki

Unatumika katika Makanisa ya Kiorthodoksi. Mkono wa kushoto unainuka, kutokana na dhana ya kuwa ndio upande wa mhalifu aliyetubu msalabani karibu na Yesu: hivyo unamaanisha ushindi wa wema dhidi yas ubaya. Herufi IC XC (C inasomeka S) ni za kawaida katika Ukristo wa Mashariki zikiwa na maana ya jina la Yesu, kwa Kigiriki Ιησούς Χριστός, Iesus Khristos.

Msalaba wa Mt. Birgita

Msalaba huu unapatikana kote nchini Ireland. Inasemekana Brigit (au Brigid, Brìghde, Brìde na Bríde) alikuwa mungu jike wa moto katika dini ya Waselti kabla ya Ukristo kuenea.

Chi-Rho

Ishara ya Konstantino Mkuu, Chi-Rho inatokana na herufi mbili ya alfabeti ya Kigiriki.

Msalaba wa Lorraine

Unatumika katika ngao ya Lorraine, Ufaransa. Inasemekana ulikuwa kwanza ishara ya Yoana wa Arc, msichana aliyeongoza mapigano dhidi ya Waingereza waliovamia nchi yake.

Msalaba wa Kimaria

Ukiwemo katika ngao ya Papa Yohane Paulo II, unasisitiza heshima ya Wakatoliki kwa Bikira Maria aliyesimama chini ya msalaba wa Mwanae huko Golgota.

Msalaba wa Kaskazini

Unatumika katika bendera za nchi za Skandinavia kama ishara ya Ukristo; nchi asili ni Denmark.

Msalaba wa Occitania

Ukitokana na ngao ya mtawala wa Toulouse, Ufaransa, umekuwa ishara ya Ufaransa Kusini nzima.

Msalaba wa Kipapa

Mbao tatu zinazokatisha mhimili wa msalaba zinamaanisha mamlaka ya Papa kama Askofu wa Roma, Patriarki wa Magharibi na mwandamizi wa Mtume Petro, mkuu wa Mitume wa Yesu.

Msalaba wa Kipatriarki

Mbao mbili zinazokatisha mhimili wa msalaba zinamaanisha mamlaka ya askofu mkuu na Patriarki katika Makanisa ya Kiorthodoksi.

Msalaba wa Kipresbiteri Unatumiwa na madhehebu ya Wakalvini.
Msalaba Mwekundu

Unatumika katika sehemu kubwa ya dunia kumaanisha shughuli za kitabibu.

Msalaba wa Sadaka

Msalaba wa Kilatini ukiwa na upanga juu yake, ncha yake ikielekea chini, unatumika katika shamba la Mungu la askari wa Jumuia ya Madola waliouawa vitani.

Msalaba wa Salem

Unachukuliwa pengine mbele ya Papa, ukiwa na ubao mmoja kuliko msalaba wa Kipatriarki, lakini upande wa chini, si wa juu kama katika msalaba wa Kipapa.

Msalaba wa Georgia

Unatumika nchini Georgia kama bendera ya taifa.

Msalaba wa Shada, Msalaba wa Mt. Nino

Unajulikana pia kama "Msalaba wa mzabibu"; inasemekana ulitumiwa kwanza na Mt. Nino, mwanamke wa karne ya 4 aliyeingiza Georgia katika Ukristo. Ni ishara ya Kanisa la Kiorthodoksi la Georgia.

Msalaba wa Nasrani Menorah Msalaba wa Mt. Thoma

Unasemekana kutumiwa kwanza na Mtume Thoma, aliyeeneza Ukristo hadi India, na unatumiwa na Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar kama ishara yake, pamoja na kwamba inaheshimiwa na Wakristo wote wa Mashariki wa nchi hiyo.[1]

Msalaba wa Mt. Andrea

Unapatikana katika bendera ya Scotland na kuitwa kwa Kilatini crux decussata. Inasemekana Mtume Andrea aliuacha juu ya msalaba wa namna hiyo.

Msalaba wa Mt. Joji

Unatumika katika bendera ya Uingereza.

Msalaba wa Mt. Petro, Msalaba uliopinduliwa

Unaitwa kwa jina la Mtume Petro kutokana na mapokeo ya kwamba alitaka kusulubiwa kichwa chini, miguu juu. Siku hizi unatumiwa na wafuasi wa dini ya Shetani kama ishara ya kumpinga Kristo.

Msalaba wa Tau, crux commissa

Unajulikana pia kama msalaba wa Antony Abati, kwa hiyo pia kama Msalaba wa Misri; unakosa upande wa juu ya msalaba, hivyo ni kama herufi T. Fransisko wa Asizi aliutumia kama saini.

Msalaba wa Wezi

Una sura ya msalaba uliotumika zamani kuua wezi ukifanana kama herufi Y. [2]

Msalaba wa Baharia

Unafanana na nanga, hivyo unatumiwa na mabaharia. Unaitwa pia kwa jina la Papa Klementi I kutokana na namna alivyouawa kwa ajili ya imani yake.

Msalaba wa Shirika la Kristo

Umekuwa kitambulisho cha Ureno, kutokana na shirika la zamani la nchi hiyo lililoitwa Shirika la Kristo.

Mikono ya Mungu

Ni ishara iliyotumiwa katika Ulaya ya Kati kabla Ukristo haujaingia.

Swastika

Ni msalaba ambao mbao zake zinalingana kwa ukubwa, halafu zina matawi 4 ya ziada kuelekea kulia au kushoto. Ulitumika tayari katika Zama za mawe na mpaka leo hasa nchini India na katika dini zilizotokea huko. Ulitumiwa pia na Adolf Hitler, na tangu hapo unachukiwa na wengi.

Fuvu la Kichwa na Mifupa

Si msalaba, ila ni ishara iliyowekwa mara nyingi upande wa chini wa msalaba.

Katika bendera

[hariri | hariri chanzo]

Bendera nyingi zinabeba ishara ya msalaba.

Bendera za nchi huru zenye msalaba

[hariri | hariri chanzo]

Bendera nyingine zenye msalaba

[hariri | hariri chanzo]
  • Chevalier, Jean (1997). "The Penguin Dictionary of Symbols". Penguin ISBN 0-14-051254-3
  • Koch, Rudolf (1955). The Book of Signs. Dover, NY. ISBN 0-486-20162-7.
  • Drury, Nevill (1985). Dictionary of Mysticism and the Occult. Harper & Row ISBN 0-06-062093-5
  • Webber, F. R. (1927, rev 1938). Church Symbolism: an explanation of the more important symbols of the Old and New Testament, the primitive, the mediaeval and the modern church. Cleveland, OH. OCLC 236708.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: