Che Guevara
Ernesto Guevara au Che Guevara (Rosario, Argentina, 14 Mei 1928; La Higuera, Bolivia, 9 Oktoba 1967 ) alikuwa tabibu mzaliwa wa Argentina aliyekuwa mfuasi wa itikadi za Kisoshalisti za Karl Marx. Guevara anajulikana zaidi kwa harakati zake za kimapinduzi dhidi ya tawala za kibepari huko Amerika ya Kusini na Afrika.
Guevara alipewa jina la "che" huko Amerika ya Kati likimaanisha "mshangao". Alitumia usafiri wa pikipiki kutoka Amerika ya Kusini hadi Amerika ya kati.
Guevara kwa sababu ya kufiwa na bibi yake aliyemuuguza kwa muda mrefu aliamua kusomea utabibu.
Wakati akisomea utabibu, Che Guevara alizunguka katika nchi mbalimbali za Amerika ya Kusini ambapo alijionea mwenyewe umaskini uliokithiri. Alisikitishwa sana na maisha ya ufukara waliokuwa wakiishi wananchi wengi, huku wachache wakiwa wanamiliki mali za nchi hizo. Alifikiria jinsi ya kuweza kubadili hali hii na kuamua kuwa njia pekee ya kuondoa umaskini na ukandamizaji ni mapinduzi. Aliamua kusoma kwa undani falsafa ya Karl Marx na baada ya hapo alijihusisha na harakati za kisoshalisti nchini Guatemala chini ya rais Jacobo Arbenzi Guzmán.
Mwisho mwa miaka ya 1950, Guevara aliungana na Fidel Castro aliyekuwa akiongoza kundi la kijeshi lililotwaa madaraka kwa nguvu nchini Kuba mwaka 1959. Guevara alikuwa mmoja wa viongozi wa serikali mpya ya Kuba. Katika kipindi hiki, Guevara aliandika vitabu na makala mbalimbali kuhusu nadharia na vitendo vya vita vya msituni kwa nia ya kuondoa madarakani tawala za kibepari na kibeberu.
Mwaka 1965 Guevara aliondoka nchini Cuba akielekea Kongo-Kinshasa (hivi sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) kwa siri kusaidia harakati za kuondoa utawala uliokuwa ukiongozwa na vibaraka wa mataifa ya Magharibi chini ya Mobutu Sese Seko baada ya kuuawa kwa Patrice Lumumba. Mmoja ya watu ambao walifanya kazi na Guevara alipokuwa nchini Kongo ni Laurent Kabila, aliyekuwa baadaya rais wa nchi hiyo.
Guevara aliondoka nchini Congo na kuelekea Bolivia ambapo alikamatwa mwaka 1967 na jeshi la Bolivia likishirikiana na majasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Jeshi lilitangaza kutoa zawadi nono kwa yeyote atakayesaidia kukamatwa kwa Che Guevara. Baada ya kukamatwa kwake, aliuawa kinyama.
Baada ya kifo chake, Guevara alichukuliwa kama nguzo ya vuguvugu la kimapinduzi ya kishoshalisti duniani. Picha yake na kofia aina ya Beret aliyopenda kuivaa, vimekuwa kama alama za mapinduzi ya mrengo wa kushoto duniani.
Viungo vya nje
hariri- Che Guevara - Alama ya harakati Archived 16 Julai 2006 at the Wayback Machine. -by Tony Saunois
- Ernesto Che Guevara at Rodovid Historia ya Che Guevara
- Picha za Guevara Archived 15 Julai 2006 at the Wayback Machine.
- marejeo ya filamu ya Motorcycle Diaries
- Picha, hotuba, maandiko ya Che Guevara
- Video za Che Guevara Archived 11 Desemba 2008 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Che Guevara kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |