Mkoa wa Tanga
5°18′15″S 38°19′3″E / 5.30417°S 38.31750°E
Mkoa wa Tanga |
|
Mahali pa Mkoa wa Tanga katika Tanzania | |
Majiranukta: 5°0′S 38°15′E / 5.000°S 38.250°E | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Wilaya | 6 |
Mji mkuu | Tanga |
Serikali | |
- Mkuu wa Mkoa | Martin Shigela |
Eneo | |
- Jumla | 27,348 km² |
Idadi ya wakazi (2022) | |
- Wakazi kwa ujumla | 2,615,597 |
Tovuti: http://www.tanga.go.tz/ |
Mkoa wa Tanga ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania na uko Kaskazini Mashariki mwa nchi, ukipakana na Kenya upande wa Kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki na mikoa ya Morogoro, Manyara na Kilimanjaro wenye Postikodi namba 21000. Mpaka upande wa kusini unafuata mto Mligaji kuutenganisha na mkoa wa Pwani.
Makao makuu yako Tanga mjini.
Eneo la mkoa
[hariri | hariri chanzo]Tanga ni kati ya mikoa midogo ya Tanzania ikiwa na msongamano mkubwa wa wakazi ndani ya eneo lake. Msongamano ni mkubwa hasa wilaya ya Lushoto kwenye ardhi yenye rutuba nzuri.
Mkoa una eneo la km² 27,348 ambalo linaunganisha sehemu za pwani pamoja na milima ya ndani kama Usambara.
Eneo linalofaa kwa kilimo ni km² 17,000.
Kuna wilaya 11 ambazo ni Bumbuli, Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini, Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini.
Hali ya hewa
[hariri | hariri chanzo]Kwa jumla hali ya hewa ni joto lenye unyevu. Handeni kuna joto kavu zaidi. Milima ya Usambara hakuna joto sana.
Miezi ya Desemba - Machi halijoto huko Tanga inafikia sentigredi 30-32 mchana na 26-29 usiku. Wakati wa Mei hadi Oktoba halijota inapoa: ni sentigredi 23-28 mchana na 20-24 usiku. Unyevu iko juu kati ya asilimia 100 na asilimia 65.
Maeneo mengi ya mkoa hupokea angalau milimita 750 za mvua kwa mwaka au zaidi. Pwani ni zaidi: takriban milimita 1,100 hadi 1,400 ikipungua sehemu za ndani isipokuwa milima ya Usambara ambako mvua inaweza kuzidi milimita 2000 kwa mwaka.
Wakazi
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 2022 wakazi waliohesabiwa katika sensa walikuwa 2,615,597 [1] kutoka 2,045,205 wa mwaka 2012[2].
Makabila makubwa mkoani Tanga ni Wasambaa, Wazigua, Wabondei na Wadigo. Mengine ni Wapare, Wataita, Wambugu, Wasegeju na Wanago.
Pia kuna Waarabu wengiwengi wenye asili ya Oman.
Wasambaa ndio kabila kubwa lililoko katika milima ya Usambara, Muheza, Korogwe na Lushoto. Kwa jumla ndio asilimia 40 ya wakazi wote wa mkoa.
Wazigua ni kabila kubwa huko Handeni na sehemu za Korogwe na Pangani. Wabondei wako hasa Muheza na sehemu za Pangani. Wadigo ndio wengi Tanga yenyewe na sehemu za pwani.
Elimu
[hariri | hariri chanzo]Katika mkoa huu elimu inahitaji kuboreshwa zaidi, hasa maeneo ya vijijini, maana watu wengi wa mkoa huu hufanya shughuli zao za kimila na kushindwa kuendelea na zile za maendeleo katika taifa la Tanzania.
Uchumi
[hariri | hariri chanzo]Wakazi wengi hutegemea kilimo cha riziki pamoja na ufugaji na uvuvi.
Mazao ya chakula hasa ni mahindi, muhogo, ndizi, maharagwe na mpunga.
- Mazao ya biashara ni katani, pamba, kahawa, chai, nazi, tumbaku na korosho.
- Mifugo ni ng'ombe, mbuzi na kondoo pamoja na kuku.
- Katani ilikuwa zao la biashara hasa kwa ajili ya Tanga tangu kuingizwa kutoka Mexico zamani za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hulimwa kote mkoani isipokuwa Lushoto, hasa Muheza na Korogwe kwenye mashamba makubwa. Mashamba hayo yalikuwa ya walowezi, yakataifishwa baada ya uhuru. Tangu kuanguka kwa sekta ya umma yamebinafsishwa tena siku hizi. Zao la katani linategemea sana soko la dunia, umuhimu wake ulirudi nyuma tangu miaka ya 1960.
Tanga ilikuwa na viwanda vingi kiasi katika miaka ya 1960 na 1970 lakini karibu vyote vimekwama kutokana na siasa ya Ujamaa na uchumi wake ulioiga mfumo wa nchi za kisoshalisti. Viwanda vichache vilivyobaki havizalishi mali kulingana na uwezo wao. Kilichobaki hasa ni kiwanda cha saruji Tanga.
Utalii umeanza kupanuka kidogo, hasa katika eneo la Pangani, Mapango ya Amboni na kituo cha Makumbusho Urithi Tanga.
Wilaya ya Handeni kuna machimbo ya madini.
Majimbo ya bunge
[hariri | hariri chanzo]Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:
- Tanga Mjini : mbunge ni Ummy Mwalimu (CCM)
- Bumbuli : mbunge ni January Makamba (CCM)
- Mlalo : mbunge ni Rashid Abdakkag Shangazi (CCM)
- Pangani : mbunge ni Jumaa Hamidu Aweso (CCM)
- Kilindi : mbunge ni Omari Mohamed Kigua (CCM)
- Mkinga : mbunge ni Dustan Kitandula (CCM)
- Handeni Vijijini : mbunge ni Mboni Mohamed Mhita (CCM)
- Muheza : mbunge ni Hamis Mohammed Mwinjuma (CCM)
- Korogwe Mjini : mbunge ni Pius Kimea (CCM)
- Korogwe Vijijini : mbunge ni Stephen Hillary Ngonyani (CCM)
- Lushoto : mbunge ni
- Handeni Mjini : mbunge ni Omary Abdallah Kigoda (CCM)
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Mkoa wa Tanga (DOA) - kuhusu mkoa wa zamani chini ya ukoloni wa Kijerumani
- Orodha ya milima ya mkoa wa Tanga
- Orodha ya mito ya mkoa wa Tanga
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://assengaonline.com/2022/11/05/matokeo-ya-sensa-2022-tanzania/
- ↑ "Population Distribution by Administrative Units, United Republic of Tanzania, 2013" (PDF). National Bureau of Statistics, Ministry of Finance, Dar es Salaam and Office of Chief Government Statistician, President’s Office, Zanzibar. Machi 2013. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo Juni 12, 2013. Iliwekwa mnamo 2017-08-22.
{{cite web}}
: More than one of|archivedate=
na|archive-date=
specified (help); More than one of|archiveurl=
na|archive-url=
specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- (Kiingereza) Tanga Region Socio-Economic Profile Archived 10 Oktoba 2022 at the Wayback Machine. (PDF)
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Tanga kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |