Nothing Special   »   [go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Mbingu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Katika wikipedia hii tunatumia neno "mbingu" zaidi kwa maana ya kidini. Kwa mbingu kama uwazi tunaoona juu ya uso wa ardhi penye mawingu, jua na nyota tazama anga

Dante Alighieri na Beatrice wakikazia macho mbingu za juu zaidi. Mchoro huu wa Gustave Doré unafuata mashairi bora ya Kiitalia, kwa jina Divina Commedia.

Mbingu ni upeo wa Mungu au miungu katika mafundisho ya dini nyingi. Mara nyingi humaanisha pia upeo wa kiroho ambako nafsi za wafu huweza kufikia baada ya kifo.

Watu walioishi zamani, wakitegemea macho yao pekee, waliona mara nyingi ya kwamba mbingu ziko juu yetu, na tukitazama anga tunaona mwanzo wa mbingu kama mahali pa Mungu.

Lakini tangu kale watu wengine waliona ya kwamba mbingu si mahali maalumu, bali zaidi hali au upeo ambao ni tofauti na mahali popote tunapojua au tunapoweza kutambua.

Anga na mbingu

[hariri | hariri chanzo]

Katika lugha ya kila siku maneno "anga" na "mbingu" mara nyingi yanatumiwa kwa maana moja: "Mawingu yanatembea angani - mawingu yanatembea mbinguni".

Lakini mbingu huwa na maana ya ziada, yaani ya kidini, kwa kutaja pia upeo wa Mungu au hali inayopita maarifa ya duniani: "hapa ninajisikia kama mbinguni" ni tofauti sana na "hapa najisikia angani".

Etimolojia

[hariri | hariri chanzo]

Kiasili "mbingu" ni uwingi wa neno "uwingu"[1] ambalo si kawaida sana tena. Uwingu linataja uwazi juu yetu, ni upeo wa mawingu. Mbingu kama uwingi wake unatokana na dhana la kuwepo kwa tabaka mbalimbali za uwingu huu, hivyo mbingu. Mataifa ya kale yaliamini kuweko kwa mbingu saba kwa sababu waliona mianga saba angani yaliyokuwa na mwendo kati ya nyota yaani Jua, Mwezi na sayari tano zilizojulikana kabla ya kupatikana kwa darubini (Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii na Zohali). Hapa waliwaza kuwepo kwa mbingu saba ilhali kila moja alikuwa na tabaka yake ya uwingu. Kupitia maandiko ya Waislamu mtazamo huu wa dunia ulisambaa katika nchi nyingi hadi Uswahilini.

  1. Charles Sacleux, Dictionnaire Swahili- Français, Paris 1939, makala "uWingu"


Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.