Nothing Special   »   [go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Mahdi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mahdi (pia mehdi; kwa Kiarabu ‏مهدي‎ - anayeongozwa) ni cheo cha mwokozi wa dunia katika imani ya Uislamu.

Kufuatana na imani hiyo mwokozi huyu atatumwa na Allah kabla ya siku za mwisho wa dunia yaani kabla ya siku ya hukumu (yawm al-qiyamah) na atasafisha dunia na kila aina ya dhambi, ukandamizaji na utawala mbaya.

Katika Qurani hakuna maelezo ya wazi juu ya kuja kwa Mahdi lakini anatajwa katika ahadith mbalimbali; isipokuwa Sahih al-Bukhari haina habari zake. Katika imani ya Waislamu wengi (hasa Washia lakini pia katika mielekeo kadhaa ya Wasunni) mahdi ina nafasi muhimu.

Mahdi anategemewa kuwa atawaongoza binadamu kumwamini Mungu na kumshinda Dajal anayetazamiwa kuwa mwovu kati ya wanadamu. Mahdi ataongozwa moja kwa moja na Allah. Waislamu wengi wanaona ya kwamba ataongoza jitihada kwa kutumia nguvu ya silaha lakini kundi la Ahmadiyya wanasisitiza kuwa jihad yake itakuwa ya kiroho tu.

Katika imani ya Washia mahdi anajulikana tayari jina lake: ni Muhammad ibn Hasan al-Mahdi aliyezaliwa tarehe 29 Julai 869 akawa imamu wa 12 wa Washia, lakini tangu mwaka 874 alifichwa na Allah mbele ya maadui zake na tangu wakati ule anaishi mafichoni (ghaiyba).

Kati ya Wasunni kuna mafundisho tofautitofauti kuhusu mahdi. Wanaokubali ahadith juu yake huamini atazaliwa katika ukoo wa mtume Muhammad na atatawala dunia pamoja na Yesu atakayerudi duniani kwa muda wa miaka 40.

Lakini Wasunni wengine hawakubali ahadith juu ya Mahdi.

Hata hivyo, imani katika ujio wa Mahdi ilikuwa na umuhimu mara kadhaa hata kati ya Wasunni. Mashuhuri alikuwa Muhammad Ahmad aliyejitangaza kuwa Mahdi mnamo mwaka 1881 akafaulu kuunda Dola la Mahdi katika Sudan.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]