Nothing Special   »   [go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Nahari (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Nahari (Eridanus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Nahari - Eridanus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji wa angakaskazi

Nahari (kwa Kilatini na Kiingereza Eridanus) [1] ni jina la kundinyota kubwa inayoonekana kwenye angakaskazi na angakusi ya Dunia yetu.

Mahali pake

Nahari - Eridanus lina umbo jembamba lakini refu sana likianza jirani ya Jabari kwenye angakaskazi hadi karibu na Wingu Dogo la Magellan katika Tukani kwenye angakusi.

Linapakana na makundinyota jirani ya ) (Tucana) , ) (Hydrus), Nyavu (Reticulum), Saa (Horologium), Patasi (Caelum) , Arinabu (Lepus), Jabari (Orion), Ng'ombe (pia Tauri, lat. Taurus), Ketusi (Cetus), Tanuri (Fornax) na Zoraki (Phoenix).

Jina

Nahari (Eridanus) lilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema النهر an-nahar kwa maana ya “mto[2]. Waarabu walitafsiri hapa jina la Ptolemaio aliyetaja nyota hizi vile kwa jina la Ποταμός potamos yaani mto katika orodha yake ya Almagesti[3].

Hatuna uhakika jinsi Wagiriki wa Kale katika mawazo yao kuhusu umbo la Dunia walivyoona Eridanus – Nahari; inaweza kumaanisha "mto" kwa maana ya jumla ya maji yaliyozunguka nchi kavu yote na maji haya waliyaita “Okeanos”, neno ambalo baadaye likawa “ocean” (Bahari kuu) katika lugha za Ulaya. Waandishi wengine wa Ugiriki ya Kale walitaja mto fulani kwa jina “Eridanus”, ama mto Po wa Italia au mto katika kaskazini ya Ulaya ulioishia katika bahari penye kaharabu .

Eridanus - Nahari ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa na Klaudio Ptolemaio katika kitabu cha Almagesti wakati wa karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [4] kwa jina la Eridanus. Kifupi chake rasmi Ukia ni 'Eri'.[5]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Alpha Eridani au Achernar ("mwisho wa nahari") Ina mwangaza unaoonekana wa mag 0.45 ikiwa umbali wa miaka nuru 144 na Dunia[6][7].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
α Achernar 0.45m 144 B3 V
β 67 Cursa 2.78m 90 B3 V
γ 34 Zaurak 2.95m 150 M0 III
θ Acamar 3.0m 163 A4 + A1
δ 23 Ran 3.52m 29 K0 IV
υ4 41 3.55m 120 B8 V
φ 3.56m 120 B8 V
χ 3.69m 50 G6 IV
τ4 16 3.70m 250 M3 III
ε 18 3.73m 10.5 K2 V
υ2 52 3.82m 200 G9 III
l 53 3.9m 110 K2 IIIb
η 3 Azha 3.89m 121 K1 III
ν 48 3.93m 1000 B2 III
ν3 43 3.97m 250 K5 III
ο1 38 Beid 4.04m 200 F2 III
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Eridanus" katika lugha ya Kilatini ni "Eridani" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Eridani, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. PAL - Glossary "Eri", tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  6. Eridanus], tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  7. ACHERNAR (Alpha Eridani), tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 215 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331