Meno
Meno ni viungo vya mwili vilivyopo mdomoni vyenye kazi ya kutafuna chakula.
Meno hupatikana kwa vertebrata (wanyama wenye uti wa mgongo). Nje ya kutafuna chakula hutumiwa pia kama silaha za kujilinda au kushambulia wanyama wengine. Wanyama kadhaa huwa na meno nje ya mdomo kwa matumizi kama silaha (mfano: tembo) yanayoweza kutumiwa pia kama vifaa vya kuchimba (mfano: nguruwe-mwitu).
Kwa binadamu meno hupatika kinywani tu. Kazi kubwa ya meno kwa binadamu ni katika umeng'enyaji wa chakula anachokula na mara chache katika kusaidia kukata vitu mbalimbali kama kutatua kitambaa au kukata kamba au waya. Binadamu ana aina mbalimbali za meno zinazomsadia kula vyakula vya aina mbalimbali kama vile vya mimea na nyama. Kwa kawaida mtu mzima huwa na meno thelathini na mbili.
Utangulizi
Umeng'enyaji wa chakula huanzia kinywani. Humo tunakitafuna kwa meno mpaka kiwe laini.
Binadamu huwa na aina mbili za meno. Tunazaliwa na mbegu za meno ya utoto yanayobadilishwa wakati wa kubalehe kwa meno ya kudumu. Kwa hiyo kuna wakaa mbili za meno.
Idadi ya meno ya utoto katika wakaa ya kwanza ni 20. Huanza kuota mtoto anapokuwa na umri wa miezi sita na kawaida yote huwa yamekwisha kuota mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili.
Idadi ya meno katika wakaa ya pili ni thelathini na mbili. Huanza kuota katika umri wa miaka sita, yakakamilika katika umri wa miaka 18-20. Lakini mwingine huota upesi au hukawia.
Aina za Meno
Umbo la meno hufuatana na kazi ambayo inayapasa kufanya. Meno yaliyopo katikati ya kila taya huwa na kingo kali za kukatia chakula. Haya huitwa meno ya kukatia au meno ya mbele (ing:incisors). (meno 8 ya kukatia, katika kila taya yapo meno 4). Meno yaliyofuata meno ya kukatia ni machonge (canine). Yapo machonge 4 kwa ujumla; katika kila taya kuna machonge 2. Kazi yake ni kurarua chakula. Meno yanayofuata machonge huitwa magego madogo (premolars) (jumla ya magego madogo ni 8; na katika kila taya yapo 4); na meno yanayoyafuata hayo huitwa magego (molars) (magego yate ni 12, na katika kila taya kuna magego 6. Magego madogo na magego ni kwa kusagia chakula. Katika wakaa wa kwanza huwa hakuna magego madogo.
Muundo wa Jino
Meno hukaa kwa uthabiti ndani ya vitundu vya mataya. Kila jino lina sehemu mbalimbali. Sehemu ambayo huonekana kinywani ni kichwa cha jino, na sehemu iliyomo ndani ya taya ni shina la jino. Karibu jino zima ni la pembe. Kichwa chake ni cha ufupa mgumu sana wenye rangi nyeupe ya kung’aa, nacho kwa lugha ya kitaalam huitwa enamel. Kazi yake ni kulinda pembe ya ndani. Pembe ya shina hulindwa na tabaka aina ya saruji ijulikanayo kwa jina la kitaalamu kama cementum.
Katikati hasa ya cementum na mfupa wa taya kuna utando, ambao unasaidia kukuza jina katika kitundu chake, nao (utando huo) hulingana na ufizi. Ndani ya jino mna mvungu wenye neva na mishipa ya damu. Neva pamoja na mishipa ya damu huingia katika mvungu penye ncha ya shina la jino.
Magonjwa ya Meno
Kuoza kwa meno
Chakula cha hatari kwa meno ni baadhi ya kile chenye asili ya unga. Kikiachwa kinywani huganda katika meno; hapo meno hupata kuwa mororo na mahali pale uharibifu utaanza. Basi vijidudu vilivyomo kinywani hushambulia mahali pale na hatimaye hutoboa kitundu. Ukubwa wa kitundu hiki utaongezeka polepole. Mwishowe kitafika mpaka mvungu wenye neva, ndipo yanapotokea maumivu makali. Hatimaye neva itaoza na kufa kabisa. Hapa maumivu hutulia kabisa. Lakini usikubali kudanganywa. Kwa njia ya mvungu hata nafasi inayozunguka ncha ya jino itashambuliwa, na vijidudu vitaenea hadi kwenye utando wa ule mfupa na hatimaye kusababisha jipu na madhara mengine kinywani.
Kiseyeye
Zaidi ya kuoza kwa meno kuna ugonjwa wa mishipa inayozunguka meno, ndiyo kiseyeye (Pyrrohoea). Katika ugonjwa huu ufizi unaweza kuvimba na kutoka damu ukiguswa kidogo tu, kama kwa mfano mtu anaposafisha meno yake kwa mswaki. Ugonjwa ukizidi ule mfupa unaozunguka jino utaharibika na jino litalegea na mwishowe hata kutoka lenyewe. Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa vitamini C mwilini.
Magonjwa mengine yanayosababishwa na meno mabovu
Licha ya magonjwa meno, hata magonjwa mengine yanaweza kutokea. Mara nyingi vijidudu vya jipu huingia moja kwa moja katika njia ya damu, au pengine usaha unaomezwa pamoja na vijidudu huweza kuanzisha ugonjwa wa kuvimba katika sehemu nyingine za mwili.
Utunzaji wa meno
Inampasa kila mtu kusafisha meno yake baada ya kula na kuondoa vipande vyote vya chakula vinavyobaki hasa kati ya jino na jino. Wakati mwingine ulio bora kwa kusafisha meno kabla ya kwenda kulala. Ili ufanikiwe kusafisha meno vizuri tumia mswaki; na ili kuondoa vipande vya chakula vilivyomo kati ya jino na jino tumia kijiti chenye ncha kali au kilichochongeka. Wakati ugonjwa wa meno unapoanza, ikiwa daktari wa meno yuko katika mtaa au kijiji chako, umwendee ili azibe tundu la jino lako. Jino lolote bovu lisiloweza kutibiwa tena inafaa ling’olewe ili lisiweze kuambukiza ugonjwa katika sehemu nyingine za mwili.
Angalia Pia
Marejeo
- Roberts, M. (2000). Advanced Biology, Nelson, London.
- Franks, A. S. T. (1973). Geriatric Dentistry, Oxford